Abstract:
Utafiti huu ulinuia kutathmini nyimbo za Kiswahili zinazotumika katika shule za chekechea kama nyenzo ya ufundishaji katika kata nne za Kaunti ya Makueni ambazo ni Mukaa, Kilungu, Kathonzweni na Makueni. Kaunti ya Makueni ina idadi ya kata tisa kwa ujumla. Kata hizi nne ziliteuliwa kwa sababu utafiti wa awali ulionyesha kwamba kwenye kata hizo kuna shule za chekechea ambazo zina mchanganyiko wa walimu na wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini Kenya na waliozungumza lugha asili tofauti. Hivyo, nyimbo za Kiswahili zilitumika katika ufundishaji katika sehemu kubwa kwa kuwa zilieleweka na wanafunzi wote. Shule saba za kiserikali na tatu za kibinafsi ambazo zenye wanafunzi wengi zilishughulikiwa katika utafiti huu. Shule mbili hadi tatu zilichaguliwa katika kila kata kulingana na idadi ya wanafunzi na maeneo ya shule hizo. Mbinu za kusudio ilitumika kuchagua nyimbo za Kiswahili ishirini na tano kwa jumla. Madhumuni ya utafiti huu ilikuwa ni; Mosi, kuainisha aina za nyimbo za Kiswahili zilizotumika kama nyenzo ya ufundishaji katika shule za chekechea nchini Kenya. Pili, kubainisha namna nyimbo za Kiswahili zilivyotumika kama nyenzo ya ufundishaji na tatu, kufafanua athari za matumizi ya nyimbo za Kiswahili kama nyenzo ya ufundishaji katika shule za chekechea. Utafiti uliongozwa na nadharia ya kiutambuzi iliyoasisiwa na Jean Piaget mwaka wa 1954. Sampuli lengwa ilikuwa ni shule saba za kiserikali na tatu za kibinafsi. Pia, mbinu ya hojaji ilitumika katika ukusanyaji wa data kutoka kwa walimu. Kwa kuwa walimu wa shule za chekechea huwa wachache, mtafiti alishirikisha walimu wote waliofundisha shule za chekechea katika kata zilizochaguliwa. Data ya utafiti huu ilichanganuliwa kwa kutumia njia ya kimaelezo na kitakwimu. Utafiti huu umebaini kwamba nyimbo za Kiswahili ni mojawapo ya nyenzo muhimu ya ufundishaji katika shule za chekechea nchini Kenya. Kwa hivyo, kila shule ya chekechea nchini ni muhimu kuzitumua katika ufundishaji.